Dar es salaam ni moja kati ya mji unaokua kwa kasi zaidi barani Afrika. Idadi ya watu inatarajiwa kukua kwa kiwango kikubwa na kwamba Dar es salaam inaweza kuwa mji wa pili kwa watu wengi zaidi duniani ifikapo mwaka 2100, kwa kuwa na idadi ya watu milioni 76, (hii ni kutokana na tafiti za  World Population Review). Kiwango cha ukuaji kwa mwaka kinatarajiwa kuwa cha wastani wa asilimia 4,36  ifikapo mwaka 2020. Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, idadi ya watu inatarajiwa kufikia million 5.

Kwa kiwango hichi cha ukuaji wa mji na zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi, usimamizi wa taka (hasa taka ngumu) ni tatizo kubwa. Vilevile kwa maendeleo ya sasa ya kijamii na kiuchumi, kiwango cha taka ngumu kimeongezeka kwa haraka sana. Kuna sera na sheria za kuongoza usimamizi wa taka katika jiji la Dar es salaam lakini hazijawahi kuwa na ufanisi, hivo watu hutupa taka hovyo na wazezavyo kwa kuwa hakuna njia sahihi ya kiufanis iliyowekwa kwa ajili ya kukusanya taka.

Mafuriko Dar es salaam husababishwa hasa na njia za maji zilizoziba kama mito, mitaro, mifereji, mito n.k. Watu hutupa taka ngumu na kusababisha njia za maji kuziba. Vitu kama vyuma, plastiki, na uchafu mwingine hutupwa na kusababisha mafuriko. Bila njia nzuri na fanisi za kusimamia taka, mafuriko yataendelea kuzidia mifumo ya mifreji ya maji na kuathiri jamii, Kwa Tabata nyumba nyingi hukumbwa na mafuriko kutokana na kuziba kwa mitaro.

Taasisi ya Humanitarian OpenStreetMap Team (HOT), na mshirika wao Openmap Development Tanzania (OMDTZ) kwa kuungwa mkono na Benki ya Dunia waliamua kufanya mradi wa majaribio wa kutengeneza ramani kwenye eneo hili lisilo rasmi (kama Tabata) sawa na vile walivyofanya katika maeneo rasmi ya jiji (Kata ya Mchafukoge na Kisutu) na kutengeneza data/taarifa ambazo zinaweza kusaidia makampuni yanayokusanya taka kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kuwafikia wateja wao

HOT na OMDTZ walishirikiana  na kampuni ya Joshemi, Kampuni inayohusika na ukusanyaji wa taka huko Tabata. Tabata ni kata iliyopo wilaya ya Ilala.Kulingana na sensa ya 2002, kata ilikuwa na jumla ya idadi ya watu 46,228. Kata hiyo inajumuisha mitaa nane (Mandela, Kisiwani, Tenge, Msimbazi Mama, Msimbazi Magharibi, Tabata, Matumbi na Mtambani). Eneo kubwa la Tabata ni makazi yasiyo rasmi na hupatikana kwenye bonde la mto wa Msimbazi (mto mkubwa unaofurika zaidi katika mji).

Kampuni ya Joshemi imetengenezwa ratiba ya wiki kwa kila mtaa ili kuweza kuchukua taka. Wakazi na wamiliki wa biashara wanatakiwa kulipa kiwango fulani cha pesa kulingana na wingi wa taka.

Lengo la zoezi hili

Kampuni ya JCL ilihiitaji kujua namba ya wateja wao, na ilikuwa ngumu sana kuwafatillia wote, mapato na mfumo bora wa kupata mrejesho kutoka kwa wateja wao kuhusu huduma inayotolewa na kampuni. Lengo ilikuwa kubadili mfumo wa analogia uliokuwa ukitumiwa na kampuni hii na kuanza kutumia mfumo wa kidigitali, pamoja na kuwatengelezea ramani zinazoonyesha wateja walipo na jinsi ya kuwafatilia. Kwa njia hii Kampuni ya JCL itaboresha huduma zao, kuongeza kipato na na kuunda utaratibu mzuri wa ukusanyaji taarifa.

Mbinu iliyotumika

RAmani ya majaribio iliyofanyika katika mitaa miwili ya Tabata (Msimbazi Mama and Msimbazi Mashariki). Kama ambavyo sera yetu imekua ya kutumia programu za wazi na huru, tumetumia programu ya  OpenDataKit (ODK) Collect na OpenMapKit (OMK) katika kukusanya taarifa ambazo ni programu huru kabisa za kwenye simu ya mkononi. Ili kurahisisha zoezi timu ilifanya kazi na wakusanya mapato kwa kuwa wanayafahamu zaidi maeneo yao.

Ukusanyaji wa taarifa. Msimbazi subward, Tabata.

Timu iliandaa mfumo wa taarifa kwenye excel ikiwa na jina la kata, jina la mtaa, mjumbe, eneo pamoja na taarifa za mteja kama jina, namba ya simu, mwezi, kiasi na ID ya risiti. Kurahisisha mchakato huu, namba bandia zilitengenezwa ili kuweza kutambua nyumba kwa kuwa kwenye makazi yasiyo rasmi nyumba hazina namba. Karatasi hii ilichapishwa na zoezi la ukusanyaji na uchakataji wa taarifa lilianza.

Namba bandia zilizowekwa ili kuweza kutambua nyumba (Hapo inaonyeshwa kwenye programu ya OMK)

Timu ikiwapa mafunzo wafanyakazi wa JCL jinsi ya kukusanya taarifa kwa kutumia ODK na OMK. Msimbazi Mama, Tabata.

Matokeo ya mradi

Kampuni hii sasa imekuwa na uelewa wa wapi wateja wao walipo, idadi na changamito wanazopata wateja. Kwa kuwa kampuni sasa inafahamu idadi ya wateja, ipo kwenye mipango ya kuoresha huduma zake kwa kuongeza magari ya taka na safari za kupeleka taka kwenye dampo. Kabla ya kupata data walikuwa wanatoa huduma kwa watu 300, baada ya ukusanyaji taarifa na data kupatikana, waligundua kuna watu 2000 wanaohitaji huduma yao. Hii haitaogeza tu kipato kwa kampuni, bali kuboresha huduma kwa wananchi na kuweka kata katika hali ya usafi.

Johanes Petro, msimamizi wa ramani kwenye shirika la OMDTZ ana mawazo chanya kuhusu mpango huu. Alikuwa na haya ya kusema,

“Mpango huu utepelekea usimamizi wa taka ulio bora, kwa kuwa kampuni inafahamu idadi ya wateja wao wanaweza hata kuongeza huduma mara mbili au mara tatu zaidi na kuhakikisha huduma bora. Kwa upande mwingine, hii itaongeza mapato kwa kampuni na kuboresha huduma kwa wananchi “. Aliongeza, “Kuna haja ya kuendeleza mchakato huu kwa makazi yote yasiyo rasmi jijini Dar es Salaam ambayo itasaidia jiji endelevu na safi kama mfumo ulioundwa ni rahisi kutumia”

Kumbuka:

Hadi sasa, timu yetu inafanya kazi na watoza mapato ili kuwawezesha katika matumizi ya data na kusaidia katika kutumia programu ya OMK kattika shuhuli zao.

Changamoto kwenye Ukusanyaji wa Taarifa

Ukusanyaji wa tarifa ulianza kwa kufanya kazi na watoza mapato, lakini wakusanya mapato walikuwa wakisita kutoa ushirikiano kwakuwa walikuwa wanategeneza risiti feki na kuibia kampuni. Hivyo waliamin kuwa, kama kampuni itapata data za wateja wote wanaohudumiwa njia zao za wizi zitagunduliwa. Hivyo hawakutoa ushirikiano mzuri na kampuni iliwafukuza.

Ilibidi kubadili mbinu na kuanza kufanya wajumbe wa shina. Viongozi hawa wanajukumu la kuongeza nyumba chache kati ya 50 hadi 200, na ni watu wa kwanza kabbisa ambao wananchi huwafuata kwa msaada unaohitaji mamlaka ya serikali. Hivyo kufanya nao kazi ni faida kubwa kwa kuwa wanafahamika na kuaminiwa na jamii.

Nini kinafuata?

Kwa matokeo haya chanya kwenye mitaa hii miwili ya majaribio, kuna haja ya kupanua mradi huu kwenye mitaa sita iliyobaki kwenye kata ya Tabata na hata kwenye jiji zima kama tutapata msaada na fedha kutoka kwa washirika tofauti. Kampuni ya Joshemi ambayo tunafanya nayo kazi wanasubiri sana kwa hamu kuona mradi huu ukifanyika kwenye kata nzima kwa kuwa sasa wanaelewa  nguvu ya data na taarifa- hata waliamua kuwalipa wajumbe waliokuwa wakisaidia katika ukusanyaji wa taarifa.

Ikiwa utaratibu huu utafanyika kwenye kata zilizobaki za jiji, ukusanyaji wa takataka utakuwa rahisi, mji utakuwa safi na pia unaweza kupunguza kiwango cha mafuriko kwa kuwa mara nyingi husababishwa na mifereji na mito iliyoziba. Pia kuna haja ya kuendeleza mfumo wa usimamizi mzuri wa gharama nafuu na unaozingatia nafasi za kiuchumi kwa ajili ya usimamizi imara wa taka kama kuchakata (recycling). Wananchi kwa ujumla pia wanahitaji kuchukua jukumu katika mchakato huu kwa kushirikiana na makampuni ya ukusanyaji taka kwa sababu faida za pande mbili. Wataalamu wetu wanafanya kazi katika kuimarisha mahusiano kati ya wateja na makampuni kwa kuwa waliona kuna mgawanyiko na matabaka kati yao.

Leave a Reply